Baada ya kelele zile Murphy alijisemea moyoni kama angebaki pale alipokuwa amebana au angetoka, washenzi wangemvua nguo; alitaka akimbilie nje lakini akasita. Nje wangeweza kumwona na hivyo kumuua wakati sasa alishaanza jitihada za kuokoa maisha yake. Alipofikiri kwa sana aliamua liwalo na liwe. Alikurupuka akajirusha nje, ambako chapuchapu alinyanyuka na kuangaza sehemu zote lakini bila kuona adui hata mmoja. Tumaini la kushinda likamwendea ghafla na kumsukuma mbele. Alikimbia mpaka kona ya kaskazini-mashariki na kubana, baada ya kusikia vishindo vya watu wakikimbia. Kwa jicho la haraka aliangalia magharibi, akaangalia tena saa na kuona kumbe alikuwa bado na muda; dakika sita wakurugenzi wangefika na upande wa magharibi hakukuwa na mtu. Murphy alishtuka baada ya kuhisi mtu karibu yake. Yule mtu alijitokeza kwa kasi, lakini ikawa bahati sana mbaya kwake. Murphy alimvuta kama mtego wa samaki, kwa mkono wake wa kushoto; akamminya kichwa kwa kidole gumba, na kumkabidhi kareti nzito ya shingo. Alipomwachia alijipiga chini kama gunia, akapoteza fahamu.
Your Comment